Kurasa za maisha: blogs list

Sunday, October 9, 2011

WANAWAKE ELLEN SIRLEAF NA WENGINE WAWILI WAPATA TUZO YA NOBEL 2011

 Oslo, Norway

WANAWAKE watatu akiwemo Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, wamepata tuzo kimataifa ya Nobel kwa mwaka huu, kufuatia juhudi zao za kutafuta amani bila fujo.

Tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu imewatunuku kwa pamoja wanawake Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Leymah Gbowee wa Liberia na Tawakul Karman wa Yemen. 

Wametambulika kutokana na "harakati zao bila kutumia vurugu kwa usalama wa wanawake na haki za wanawake katika kushiriki kikamilifu kwenye kujenga amani".

Bi Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, Bi Gbowee mwanaharakati wa amani Liberia na Bi Karman kiongozi wa harakati za kidemokrasia Yemen.

Tuzo hiyo ikitangazwa Oslo, mwenyekiti wa kamati ya Nobel Thorbjorn Jagland alisema: " Hatuwezi kufanikiwa kupata demokrasia na amani ya kudumu katika dunia hii mpaka wanawake wafanikiwe kupata fursa sawa na wanaume ili kuweza kuchochea maendeleo katika viwango vyote vya jamii."

Taarifa hiyo ilisema "ni matumaini ya kamati ya Nobel ya Norway kuwa tuzo hiyo itasaidia kumaliza ukandamizaji wa wanawake ambao bado unaendelea katika nchi nyingi, na kutambua uwezo mkubwa wa demokrasia na amani ambao wanawake wanaweza kuwakilisha."

'Bi Karman Mwanamke Ngangari'

Bi Karman anaongoza shirika la Yemen la Women Journalists without Chains, yaani waandishi wa habari wa kike wasio na mipaka na amefungwa jela mara nyingi kutokana na kampeni zake za kutaka uhuru wa habari na upinzani wake kwa rais wa serikali ya Ali Abdullah Saleh.

Alitambuliwa kwa kuchukua nafasi kubwa kwenye harakati za haki za wanawake katika machafuko ya kuunga mkono demokrasia huko Yemen "katika hali ngumu sana".

Bi Karman, mama mwenye watoto watatu, ameiambia idhaa ya Kiarabu ya BBC kuwa anatunukia tuzo yake kwa "wote waliojitoa mhanga na kujeruhiwa na machafuko ya nchi za kiarabu"- wimbi la ghasia lililoenea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kwa " watu wote wanaopigania haki zao na uhuru wao".

Ni mwanamke wa kwanza wa kiarabu kushinda tuzo ya amani ya Nobel.

Bw Jagland amesema ukandamizwaji wa wanawake ndilo "jambo muhimu sana" katika dunia ya kiarabu na kumtunukia Bi Karman ni "kutoa ishara kwamba kama itafanikiwa katika jitihada za kuleta demokrasia, lazima iwahusishe wanawake".

Bi Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ambaye tetesi kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikimwelekeza yeye, alisema tuzo hiyo ni " kwa Waliberia wote" na kutambuliwa kwa " miaka mingi ya harakati za kupata haki".
Alichaguliwa mwaka 2005, kufuatia kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 250,000, na kusababisha wengi kukimbilia nchi za nje na kuvuruga uchumi wa nchi hiyo.

Alipoingia madarakani, mchumi aliyepata elimu yake Marekani na aliyekuwa waziri wa fedha- anayejulikana kama "mwanamke Ngagari" wa Liberia aliahidi kupambana na rushwa na kuleta "hisia za kimama kwenye urais" kama njia ya kuponyesha majeraha yaliyotokana na vita.

Ni maarufu sana miongoni mwa wanawake na wasomi wachache nchini humo, lakini anachukiwa na jamii za kimila zinazoongozwa zaidi na wanaume.

Bi Sirleaf anagombea tena urais wiki ijayo, licha ya kusema kuwa atashikilia nafasi hiyo ya urais kwa mhula mmoja tu.

Taarifa kuhusu tuzo hiyo ilisema, " Tangu wakati huo amaefanya kazi ya kuwashawishi wanawake Afrika Magharibi wakati na baada ya vita."

Wanawake hao watagawana zawadi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5.

Wanawake hao walitangazwa jana na Kamati ya Nobel iliyokutana mjini Oslo, Norway.

Bi Tawakul Karman, Rais Ellen Johnson Sirleaf na Bi Leymah Gbowee///BBC
Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ni mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia kuwa mkuu wa nchi. Ujasiri wake wa kisiasa na kutopenda masihara kumemfanya apachikwe jina la “Iron Lady”.

 GBOWEE  MWANAMKE SHUPAVU
Gbowee ni mtetezi wa masuala ya amani.

Bi Gbowee alikuwa kinara wa kupinga vurugu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia, akiwashawishi wanawake wa makabila na dini zote katika harakati za amani- wakati fulani hata "kugoma kufanya ngono"- na kuwahimiza kushiriki kwenye uchaguzi.


Noble Prize LOGO










Historia ya Ellen Johnson-Sirleaf
Ellen Johnson-Sirleaf alizaliwa Oktoba 29 mwaka 1938 nchini Liberia na amekuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika mashirika ya kimataifa. Baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard, alifanya kazi katika serikali ya Rais William Tolbert mwaka wa 1970 akiwa ni Waziri wa Fedha.

 Mwaka 1985 Sirleaf alihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela baada ya kuushutumu utawala wa kijeshi wan chi yake akiwa katika kampeni za kugombea ubunge.
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf
Alitumikia kifungo hicho kwa muda mfupi na  baadaye aliwaachiwa huru kabla ya  kukimbilia uhamishoni ambako aliishi hadi mwaka 1997 aliporejea Liberia, akiwa anafanyia kazi Benki ya Dunia na Citibank.
Sirleaf alimuunga mkono kiongozi wa zamani wan nchi hiyo, Charles Taylor, katika mapinduzi yake dhidi ya Jenerali Samuel Doe, lakini baadaye aligeuka na kuwa mpinzani wake mkubwa.

Mwaka 1997 aliamua kuwania urais wa Liberia ili kumuonyesha Taylor kuwa alikuwa hamuungi tena mkono hatua illiyosababisha aandamwe na  kufikishwa mahakamani kwa madai ya kuhusika na njama za uhaini dhidi ya serikali.

Uchaguzi wa urais mwaka 2005 ulirudiwa baada wagombea urais kutopata kura za kutosha.
Katika raundi ya kwanza Sirleaf alikuwa wa pili. Mgombea wa kwanza alikuwa mpinzani wake mkubwa George Weah.

Katika raundi ya pili ya uchaguzi huo, Sirleaf alitangazwa kuwa mshindi. Hata hivyo, George Weah aliwasilisha malalamiko katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

__________________________________________________________________
BBC/ Reuters

No comments:

Post a Comment