Kurasa za maisha: blogs list

Friday, October 14, 2011

MWALIMU NYERERE MSHUMAA ULIOZIMIKA AFRIKA

 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni baba wa Taifa la Tanzania.
Baba wa Taifa Mwalimu J.K Nyerere

Mwalimu alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania,  Alizaliwa katika kijiji cha Butiama, mkoani Mara pembezoni mwa Ziwa Nyanza (sasa Victoria)  tarehe 13 Aprili, 1922. Alifariki dunia  tarehe 14 Oktoba, 1999.
Aliiongoza Tanzania toka mwaka 1961 hadi mwaka 1985.

Yeye ni mwasisi wa itikadi ya UJAMAA na KUJITEGEMEA na Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu, Kazi hii ndiyo ilimpatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la "Mwalimu."

Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiyari baada ya kutawala kwa muda mrefu. Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na ushawishi  mkubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
 

Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 ( katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika). Alikuwa mmojawapo kati ya watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki.

Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba yake; katika umri wa miaka 12 aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora. Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.

Mapadre wakatambua juhudi zake katika elimu wakamsaidia kusoma ualimu huko chuo kikuu cha  Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 - 1945.Julius Nyerere alipokuwa Makerere akaanzisha tawi la Umoja wa wanafunzi Watanganyika pia alijihusisha na uundwaji wa tawi la Tanganyika African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akafundisha  shule ya St.Mary´s.

Mwaka 1949 alipata ufadhili (Scholarship) kwenda kusoma  Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskoti   Uingereza akasoma shahada ya uzamili  katika  historia na uchumi. Alikuwa mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu nchini Uingereza na mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.

Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake
 
Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam.  Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa raisi wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere. Mwaka 1954 alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari ni chama kikuu cha siasa kinachoongoza Tanganyika.

Uwezo wa mwl. Nyerere uliwashitua uongozi wa kikoloni na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu.

Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya. Alijiuzuru ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika kupigania uhuru.

Mwalimu Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship council na Fourth committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa kidiplomasia  na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila kumwaga damu.

Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo bwana Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.

Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9/12/1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa kwanza wa jamhuri ya Tanganyika.

Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.

Nyerere akichanganya ardhi ya Zanzibar na Tanganyika wakati wa muungano 1964


Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU katika  kuungana na chama tawala cha Zanzibar ASP (Afro-shiraz Party)  na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake.
Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi 1985 alipomwachia nafasi raisi wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi.


Mwalimu Aliendelea kuongoza Chama cha Mapinduzi hadi mwaka 1990 na kuwa ushawishi mkubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.

Inasadikika kuwa Nyerere alishawishi uteuzi wa Benjamini W. Mkapa kama mgombea wa urais katika uchaguzi  mwaka 1995, na ambaye ndiye aliyechaguliwa kuwa rais katika uchaguzi huo.

Nyerere alikaa muda mwingi nyumbani kwake Butiama akijihusisha na kilimo. Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake; mwaka 1996 alikuwa mpatanishi wa pande zinazokinza, katika vita ya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.

Tarehe14 oktoba .1999 alifariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London  Uingereza, baada ya kusumbuliwa na tatizo la saratani ya damu (leukemia) , iliyosababisha mauti yake.

MAFANIKIO YAKE

  • kujenga umoja wa Taifa na utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, 
  • kushinda ubaguzi wa rangi, na juhudi zake kuchangia Taifa la Afrika kusini huru.
  • kutetea usalama wa taifa katika vita vya kagera dhidi ya Nduli Iddi Amin
  • Kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za kusini mwa Afrika, kama; Zimbabwe {ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo)

CHANGAMOTO

Siasa zake za ujamaa zilishindwa baada ya mwaka 1976. Baada ya kuona kuwa uchumi wa Tanzania hautaweza kusimama kwa siasa za kijamaa,  na yeye kutoweza kuvumilia kuendesha nchi kwa siasa ambazo yeye hakuwa muumini, Nyerere kwa maamuzi yake mwenyewe aliamua kustaafu nafasi ya urais. na kuruhusu kufanyika uchaguzi mwaka 1985, uchaguzi ambao ulimsimamisha  Ali Hassan Mwinyi  kuwa Rais, ambaye alitawala kwa siasa za uchumi wa soko huria.

 UKOSOAJI DHIDI YAKE

  • Mwl.Nyerere analaumiwa kwa siasa zake za kiujamaa kuwa zilichelewesha maendeleo ya Uchumi wa Tanzania.
    Mwalimu Julius K  Nyerere


Pia kuna makundi ya waislamu wanaomtuhumu kwa kuendesha kwa siri vita dhidi ya uislamu na upendeleo wa elimu na madaraka kwa wakristo.   

  

SIFA ZAKE           

Pamoja na changamoto na matatizo;

  • mwalimu kamwe hawezi kusahaulika kwa  juhudi zake za kujenga umoja na mshikamano kwa watanzania, ambao ndio msingi wa amani tunayojivunia sasa.
                     
  • Bado anakumbukwa na watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu na ubinadamu. 
  • Pia ataendelea kukumbukwa barani Afrika, hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.

  • Mwalimu ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwake  miaka zaidi ya 24.

  • Mwalimu ni mfano wa kuigwa kama kiongozi aliyefuata misingi ya maadili ya uongozi
    na mzalendo wa nchi hii.

Mwishoni mwa maisha yake Mwalimu Nyerere aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama.

Tarehe 14 Oktoba, 1999 mauti yalimkuta, kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu (Leukemia). Alizikwa sehemu alikozaliwa kijijini Butiama, mkoa wa Mara Mashariki mwa ziwa Victoria. Mwalimu aliacha mjane, watoto na wajukuu.       

kaburi la Nyerere kijijini Butiama

HAKIKA TUTAENDELEA KUMKUMBUKA  HAYATI MWALIMU NYERERE.



MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI.

AMINA.











Sunday, October 9, 2011

WANAWAKE ELLEN SIRLEAF NA WENGINE WAWILI WAPATA TUZO YA NOBEL 2011

 Oslo, Norway

WANAWAKE watatu akiwemo Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, wamepata tuzo kimataifa ya Nobel kwa mwaka huu, kufuatia juhudi zao za kutafuta amani bila fujo.

Tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu imewatunuku kwa pamoja wanawake Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Leymah Gbowee wa Liberia na Tawakul Karman wa Yemen. 

Wametambulika kutokana na "harakati zao bila kutumia vurugu kwa usalama wa wanawake na haki za wanawake katika kushiriki kikamilifu kwenye kujenga amani".

Bi Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, Bi Gbowee mwanaharakati wa amani Liberia na Bi Karman kiongozi wa harakati za kidemokrasia Yemen.

Tuzo hiyo ikitangazwa Oslo, mwenyekiti wa kamati ya Nobel Thorbjorn Jagland alisema: " Hatuwezi kufanikiwa kupata demokrasia na amani ya kudumu katika dunia hii mpaka wanawake wafanikiwe kupata fursa sawa na wanaume ili kuweza kuchochea maendeleo katika viwango vyote vya jamii."

Taarifa hiyo ilisema "ni matumaini ya kamati ya Nobel ya Norway kuwa tuzo hiyo itasaidia kumaliza ukandamizaji wa wanawake ambao bado unaendelea katika nchi nyingi, na kutambua uwezo mkubwa wa demokrasia na amani ambao wanawake wanaweza kuwakilisha."

'Bi Karman Mwanamke Ngangari'

Bi Karman anaongoza shirika la Yemen la Women Journalists without Chains, yaani waandishi wa habari wa kike wasio na mipaka na amefungwa jela mara nyingi kutokana na kampeni zake za kutaka uhuru wa habari na upinzani wake kwa rais wa serikali ya Ali Abdullah Saleh.

Alitambuliwa kwa kuchukua nafasi kubwa kwenye harakati za haki za wanawake katika machafuko ya kuunga mkono demokrasia huko Yemen "katika hali ngumu sana".

Bi Karman, mama mwenye watoto watatu, ameiambia idhaa ya Kiarabu ya BBC kuwa anatunukia tuzo yake kwa "wote waliojitoa mhanga na kujeruhiwa na machafuko ya nchi za kiarabu"- wimbi la ghasia lililoenea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kwa " watu wote wanaopigania haki zao na uhuru wao".

Ni mwanamke wa kwanza wa kiarabu kushinda tuzo ya amani ya Nobel.

Bw Jagland amesema ukandamizwaji wa wanawake ndilo "jambo muhimu sana" katika dunia ya kiarabu na kumtunukia Bi Karman ni "kutoa ishara kwamba kama itafanikiwa katika jitihada za kuleta demokrasia, lazima iwahusishe wanawake".

Bi Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ambaye tetesi kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikimwelekeza yeye, alisema tuzo hiyo ni " kwa Waliberia wote" na kutambuliwa kwa " miaka mingi ya harakati za kupata haki".
Alichaguliwa mwaka 2005, kufuatia kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 250,000, na kusababisha wengi kukimbilia nchi za nje na kuvuruga uchumi wa nchi hiyo.

Alipoingia madarakani, mchumi aliyepata elimu yake Marekani na aliyekuwa waziri wa fedha- anayejulikana kama "mwanamke Ngagari" wa Liberia aliahidi kupambana na rushwa na kuleta "hisia za kimama kwenye urais" kama njia ya kuponyesha majeraha yaliyotokana na vita.

Ni maarufu sana miongoni mwa wanawake na wasomi wachache nchini humo, lakini anachukiwa na jamii za kimila zinazoongozwa zaidi na wanaume.

Bi Sirleaf anagombea tena urais wiki ijayo, licha ya kusema kuwa atashikilia nafasi hiyo ya urais kwa mhula mmoja tu.

Taarifa kuhusu tuzo hiyo ilisema, " Tangu wakati huo amaefanya kazi ya kuwashawishi wanawake Afrika Magharibi wakati na baada ya vita."

Wanawake hao watagawana zawadi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5.

Wanawake hao walitangazwa jana na Kamati ya Nobel iliyokutana mjini Oslo, Norway.

Bi Tawakul Karman, Rais Ellen Johnson Sirleaf na Bi Leymah Gbowee///BBC
Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ni mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia kuwa mkuu wa nchi. Ujasiri wake wa kisiasa na kutopenda masihara kumemfanya apachikwe jina la “Iron Lady”.

 GBOWEE  MWANAMKE SHUPAVU
Gbowee ni mtetezi wa masuala ya amani.

Bi Gbowee alikuwa kinara wa kupinga vurugu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia, akiwashawishi wanawake wa makabila na dini zote katika harakati za amani- wakati fulani hata "kugoma kufanya ngono"- na kuwahimiza kushiriki kwenye uchaguzi.


Noble Prize LOGO










Historia ya Ellen Johnson-Sirleaf
Ellen Johnson-Sirleaf alizaliwa Oktoba 29 mwaka 1938 nchini Liberia na amekuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika mashirika ya kimataifa. Baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard, alifanya kazi katika serikali ya Rais William Tolbert mwaka wa 1970 akiwa ni Waziri wa Fedha.

 Mwaka 1985 Sirleaf alihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela baada ya kuushutumu utawala wa kijeshi wan chi yake akiwa katika kampeni za kugombea ubunge.
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf
Alitumikia kifungo hicho kwa muda mfupi na  baadaye aliwaachiwa huru kabla ya  kukimbilia uhamishoni ambako aliishi hadi mwaka 1997 aliporejea Liberia, akiwa anafanyia kazi Benki ya Dunia na Citibank.
Sirleaf alimuunga mkono kiongozi wa zamani wan nchi hiyo, Charles Taylor, katika mapinduzi yake dhidi ya Jenerali Samuel Doe, lakini baadaye aligeuka na kuwa mpinzani wake mkubwa.

Mwaka 1997 aliamua kuwania urais wa Liberia ili kumuonyesha Taylor kuwa alikuwa hamuungi tena mkono hatua illiyosababisha aandamwe na  kufikishwa mahakamani kwa madai ya kuhusika na njama za uhaini dhidi ya serikali.

Uchaguzi wa urais mwaka 2005 ulirudiwa baada wagombea urais kutopata kura za kutosha.
Katika raundi ya kwanza Sirleaf alikuwa wa pili. Mgombea wa kwanza alikuwa mpinzani wake mkubwa George Weah.

Katika raundi ya pili ya uchaguzi huo, Sirleaf alitangazwa kuwa mshindi. Hata hivyo, George Weah aliwasilisha malalamiko katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

__________________________________________________________________
BBC/ Reuters