Uchaguzi wa Igunga ambao ulikuwa na ushindani mkubwa wa vyama vya siasa, ulifanyika Oktoba 2 na Dk Dalaly Peter Kafumu wa CCM alitangazwa rasmi Oktoba 4 kuwa mshindi, matokeo ambayo, yalipingwa na Chadema ikituhumu mchezo mchafu wa chama hicho tawala.
Jana, akisoma matokeo ya awali ya mchakato huo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa (TACCEO), Martina Kabisama alisema: “Tulielezwa na msimamizi Uchaguzi wa Jimbo la Igunga kuwa takwimu zitakazotumika ni zile zilizotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Idadi ya wapigakura walioandikishwa ni 177, 077, lakini Oktoba 3 mwaka huu tulisomewa idadi ya wapigakura kuwa ni 171,019”.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa, tofauti ya idadi kwa walioandikishwa ni 6,058, hivyo wanaomba Tume ya Uchaguzi iwasaidie taarifa ni lini daftari la kudumu la wapigakura liliboreshwa.
Kabisama alifafanua kwamba kutokana na takwimu hizo kutofautiana, watu waliokuwa na vitambulisho vya kupigakura katika vituo mbalimbali walirejeshwa nyumbani baada ya majina yao kutoonekana kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
Akitaja takwimu za watu waliorudishwa, Kabisama alisema katika Kituo cha Shule ya Msingi Nanga, watu 15 walirudishwa, wawili katika Kata ya Mgondavile, Kata ya Mbutu wawili na Nyandekwa watu wawili pia.
Kituo kingine kilichokumbwa na mkasa huo ni cha Bulyang’ombe kilichopo Kata ya Nanga ambako mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Ngole, alizuiliwa kupiga kura kwa madai kwamba, kumbukumbu zake katika daftari la kudumu la mpigakura zinaonyesha amefariki dunia.
![]() |
| Aliyekuwa kamishina wa madini Dr. Dalali Kafumu, ambaye ndiyo mbunge mpya jimbo la Igunga. |
Uvunjwaji wa haki za binadamu
Katika hatua nyingine, waangalizi hao walitaja vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kuwa ni miongoni mwa matukio yaliyojitokeza wakati wa kampeni hadi kutangazwa kwa matokeo. Kabisama alitoa mfano wa vurugu zilizotokea Oktoba 3 mwaka huu katika Hoteli ya Kilimanjaro Lodge, saa 4:00 asubuhi.
Alisema katika vurugu hizo, wafuasi wa chama kimoja cha siasa waliokuwa wamevalia sare za kijani na njano, walionekana wakitumia silaha za jadi kama mapanga, pinde, mishale, visu, fimbo na rungu wakipambana na wenzao waliokuwa wamevaa kiraia ambao walitumia mawe, huku mmoja wao akijihami kwa kuonyesha bastola.
Alitaja matukio mengine kuwa, ni kudhalilishwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatuma Kimario, mtu mmoja kumwagiwa tindikali na watoto wadogo kuvalishwa skafu za vyama na kutangulizwa kwenye maandamano yaliyoambatana na fujo.
Kampeni siku ya uchaguzi
Katika matokeo hayo, Kabisama alisema waangalizi hao walishuhudia watu wakifanya kampeni siku ya uchaguzi katika eneo la Ibutamashuzi Kata ya Mbutu, watu waliyosaidkiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, walihamasisha watu wampigie kura mgombea wao.
Katika Kituo cha Mwamashiga, msimamizi wa kituo aliyekuwa mratibu wa uchaguzi alitoka nje na kusema mgombea wa CCM Kafumu hana mpinzani.
Alisema wakati hayo yakiendelea, katika Kata ya Ngulu, waangalizi hao waliona gari alilokuwa amepanda mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu likifukuzana na gari alilokuwa amepanda mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage.
Alisema gari hilo lilikuwa na vipaza sauti na lilikuwa likitangaza kuwa mgombea ubunge kupitia Chadema, Joseph Kashindye amejitoa kwenye uchaguzi na kuwataka watu kuchagua CCM.
Matumizi ya Teknohama
Kabisama alibainisha kwamba, eneo hilo bado halina rasilimali za kutosha kuwezesha uchaguzi na matokeo yake kutangazwa kwa wakati.
“Kwa kuwa ulikuwa uchaguzi wa Jimbo moja, tulitarajia kuwa matokeo yangetolewa kwa muda mfupi, lakini yalichelewa kiasi cha kusababisha hisia na vurugu kwa wafuasi walioandamana katika eneo la kuhesabia kura,"alisema Kabisama.
______________________________________________________
Mwananchi tz

No comments:
Post a Comment